Siku mbili tu baada ya kifo cha mwanaume mweusi (mwafrika) ambaye video ya kukamatwa kwake iliwekwa mtandaoni na mpita njia, kumezuuka taharuki jijini Minneapolis, jimbo la Minnesota, Marekani.

Kwenye video, afisa wa polisi mzungu anaonekana akiwa amemkamatia chini marehemu George Floyd huku goti la afisa huyo likiwa limembana shingoni akiboboja na kuomba aachiliwe. Maandamano yamezuka jijini Minneapolis yenye jumbe za kutaka maafisa waliohusika kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

Akiwahutubia waandishi wa habari Jumatano, Meya wa jiji la Minneapolis Jacob Frey amemtaka mwanasheria mkuu wa Kaunti ya Hennepin achukue hatua za haraka za kumfikisha mahakamani afisa mhusika mkuu kulingana na ushahidi uliopo.

“Kwa nini muuaji wa George Floyd hayuko kwenye jela? Ingekuwa ni wewe au mimi nilitenda kitendo hiki, ningekuwa korokoroni hivi sasa. Sina jibu mwafaka kwa swali lako,” Frey aliwaeleza wanahabari Jumatano.

“Sote tumetazama video ya dakika tano nzima za uchungu usiomithilika ambapo afisa amemfinyilia shingo barazani mwanaume mweusi aliyetiwa pingu za mikono nyuma kwa goti,” Meya aliongezea, na kutaja kwamba mbinu hiyo ya kukabili mshukiwa ni marufuku katika idara ya polisi. “Kwa hakika sikuona hatari; sikuona chochote ambacho kingemfanya afisa huyu kutumia nguvu kiasi kile.”

Hata hivyo bwana Frey hakubainisha ni mashtaka gani angependa mhusika ayajibu na kuongeza kwamba asingependa kuingilia uchunguzi kwa matamshi. Kwenye mahojiano ya runinga mapema Jumatano, ndugu wa kike wa marehemu Bi. Bridgett Floyd alisema,
“Ningependa wale maafisa waliohusika kushtakiwa kwa mauaji kwa sababu kitendo chao kilikuwa cha kuua. Walimuua ndugu yangu; huku akilia kwi kwi kwi akiomba wamwachilie.”

Alisema kwamba licha ya familia kupata mawakili, hawajaridhika na tangazo kwamba wahusika wamepigwa kalamu – jambo ambalo Meya Frey anasema ni hatua nzuri. Idara ya Polisi ya Jiji la Minneapolis haijafichua majina ya maafisa hao, lakini imetaja kwamba makachero wa FBI pia wanachunguza mazingira ya kifo cha Ndugu Floyd.

Tangazo hili halikuwaridhisha waandamanaji ambao Jumatano jioni walifurika nje ya ofisi za Idara ya Polisi wakiimba “Hakuna Amani Bila Haki”. Baadaye makabiliano makali yakazuka. Maafisa wa kukabiliana na ghasia walitumia risasi za plastiki na vitoa machozi kuwatawanya waandamanaji waliokuwa na hamaki.

Wakenya wengi wanaoishi katika jimbo la Minnesota wana hofu kwa hali hii ya mambo.

“Watoto wa kiume wanaozaliwa hapa wana mstakabali mgumu kama hali hii itaendela hapa Marekani”, amesema mkenya mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe.
“Tunachosubiri ni kuona kama haki itatendeka. Itavunja moyo sana kama chochote hakitatokea.” Aliongezea Grace Marucha – mkenya anayeishi viungani mwa jiji la Minneapolis.

Kilichofanyika Minneapolis si kigeni Marekani. Mapema mwaka huu katika jimbo la Georgia, kijana mmoja mwafrika aliandamwa na wanaume wawili wazungu – baba na mwanawe – na kupigwa risasi kadhaa alipokuwa akifanya mazoezi ya kukimbia mtaani. Wahusika hawakukamatwa mpaka video ilipozuka mitandaoni baada ya miezi kadhaa.
Wiki jana tu kulizuka video nyingine mtandaoni katika bustani ya jiji la New York ambayo ilizua gumzo kwenye mitandao ya kijamii. Kwenye hiyo video, mwanamke mzungu anapigia polisi simu alipoombwa na bwana mmoja mwafrika amvute mbwa wake.
“Ananirekodi na kunitisha mimi na mbwa wangu,” anasikika akiwaeleza polisi kwenye 9-1-1 ingawa huyu bwana alikuwa mtulivu kabisa.

Baada ya video kuibuka, mwanamke huyo alifutwa kazi na mwajiri wake – kampuni ya Franklin Templeton.

Video ya mauaji ya Floyd, inaleta kumbukumbu za mauaji mengine sawia yaliyotokea New York miaka michache iliyopita. Itakumbukwa kwamba mwathiriwa wakati huo (2014) ni mwafrika mwingine kwa jina Eric Garner ambaye alikata kamba alipokabwa kooni na afisa mwingine mzungu licha ya kusalimu amri kwa maneno: “I can’t breathe” [Siwezi Kupumua].

Floyd pia anasikika akilia kwa uchungu mara kadhaa akiwa amesukumwa chini barazani, mikono yake ikiwa na pingu na afisa wa polisi akimpigia goti shingoni. Watazamaji na wapita-njia wanasikika wakimrai afisa amwachilie kwa sababu Floyd alikuwa hoi na akitokwa na damu puani ishara ya kukata roho. Ombi hili halikuwahusu ndewe wala sikio afisa huyu na wenzake wakati wote mpaka masiki Floyd akajinyamazia. Huyu afisa hakubandui goti lake mpaka wahudumu wa afya walipofika na ambulensi na kumbeba Floyd kwa machela.
Ikumbukwe kwamba yule afisa wa New York aliyemkaba Garner, bwana Daniel Pantaleo, hakushtakiwa kwa kosa lolote lakini alifutwa kazi mwaka jana baada ya jaji kutoa pendekezo hilo.

Maandamano yanayoendelea Minneapolis huenda yakaweka maisha ya waandamanaji – wengi wao wakiwa waafrika – katika hatari ya kuambukizwa Virusi vya Korona na kusababisha athari zaidi kwa jamii hii inayobaguliwa kirangi hapa Marekani.

Makala ya Jonah Ondieki

Positive SSL

Enjoy this blog? Please spread the word :)